Wanafunzi wa Elimu ya Juu watumia vyeti feki vya vifo kuombea mikopo
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imebaini kuwepo kwa baadhi ya wanafunzi ambao wamewasilisha vyeti feki vya vifo vya wazazi wao ili waonekane kama ni watoto yatima huku wakihitaji kupewa kipaumbele cha kupatiwa mkopo.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru, aliliambia gazeti la Habari leo kuwa wahusika wote ambao wamewasilisha vyeti hivyo feki suala lao limekabidhiwa kwa mamlaka zinazoshughulika na makosa ya jinai.
Mkurugenzi huyo hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo kwa maelezo kuwa bado wanaendelea na ukaguzi.
“Bado tunaendelea kuchunguza na idadi yao hapa sina, tukikamilisha tutawaita kuwaambia idadi yao. Kutokana na kasoro hizo, ndio maana kuna baadhi ya watu wanaolalamika kuwa ni yatima, lakini hawakupata mkopo,”
“Hayo malalamiko ya kwamba kuna yatima wamekosa mikopo tumeyasikia, lakini na sisi tunajiridhisha kuwa huyu ni yatima baada ya kupata uthibitisho wa vyeti vya vifo kutoka Rita,” alisema Badru.
Aidha Badru alisema kuwa baadhi ya wanafunzi ambao wanalalamika kuwa wamekosa mikopo ni wale ambao maombi yao yalikaguliwa na kukutwa na dosari kadhaa, na wakaombwa wazirekebishe kasoro hizo, lakini baadhi yao hawakufanya hivyo.
Kuwepo kwa vyeti hivyo vya bandia kumegunduliwa na bodi hiyo baada ya kupeleka nakala za vyeti vyote vya vifo ofisi ya Msajili wa Vizazi na Vifo (Rita) kwa ajili ya uthibitisho ndipo ikagundulika kuwepo kwa kasoro hizo.
BY: EMMY MWAIPOPO
0 comments:
Post a Comment