PICHA: TAZAMA KUKU HAWA WENYE NGOZI NYEUSI
AINA kadhaa za kuku weusi hupatikana barani Asia, lakini kuku au ndege aina ya Silkie wa huko China, ndiyo maarufu zaidi. Ndege hao, kama majina yao yalivyo, huwa wana manyoya yanayofanana na hariri.
Hata hivyo, chini ya uzuri wote huo, ndege hao wana ngozi nyeusi tii! Ndege hao huuzwa katika nchi za magharibi kama mapambo, ambapo nchini China ni kitoweo cha hali ya juu kwani nyama yake hupendwa sana. Pia ndege hao huchukuliwa kama ‘mama wema’ kwani wanaweza kuatamia mayai ya ndege wengine bila kinyongo.
Wachina huwaelezea ndege hao kama “kuku wenye mifupa myeusi” au “wu gu ji” na wamekuwa wakiwala kwa kuamini nyama yao ina tiba tangu karne ya saba au ya nane ambapo wanawake huila kwa ajili ya kuimarisha afya zao baada ya kujifungua. Pia nyama hiyo inaaminika kuimarisha mapafu, tumbo na damu ikiliwa. Wachina huitumia nyama ya ndege hao kwa kutengeneza supu yake na kuichanganya na viungo na matunda mbalimbali kwa ajili ya tiba.Utafiti uliofanywa na kuchapishwa mwaka 2011 ulionyesha kwamba hali hiyo ya kipekee ya ndege hao aina ya Silkie ambayo inajulikana kama ‘fibromelanosis’ inatokana na mabadiliko katika jeni. Mabadiliko hayo kisayansi huenda sambamba na kuongezeka kwa chembechembe za rangi ambazo huzifanya sehemu za ndani (mwilini) na mifupa kuwa nyeusi.
Ndege hao pia wana chembechembe za aina ya ‘carnosine’ ambazo huongeza nguvu mwilini. Watu wenye kutaka kuongeza ukubwa wa misuli huwatumia kwa wingi kwa nia hiyo na kama chakula chenye kuleta nguvu. Pia hutumika katika kupambana na ugonjwa wa akili wa watoto (autism), kisukari na kupambana na matatizo yanayotokana na uzee.
Kwa jumla ndege hao hutumiwa kama tiba ya maumivu ya viungo na kuzuia ugonjwa wa akili ujulikanao kama Alzheimer.
Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi kuhusu kuku nchini Uingereza, mayai ya kuku weusi ni bora kwa afya hasa yakitumika katika kupika keki. Yakilinganishwa na mayai mengine, mayai ya kuku weusi yana kiwango kidogo cha tindikali katika mafuta yake. Kwa waliowahi kuila nyama yake, wanasema ina ladha kama ya kuku wa kawaida, lakini baadhi hudai ni tamu zaidi. Je, ungependa kula nyama ya Silkie ili ufahamu utamu wa nyama nyeusi?
0 comments:
Post a Comment